TAFAKARI YA SIKU JUMATATU YA JUMA LA 4 LA MWAKA 04/02/2019

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU

JUMA LA NNE MWAKA C WA KANISA-TAREHE 04.02.2019

SOMO LA 1. EBR 11:32-40

INJILI. MK 5:1-20

FUNDISHO KUU: SHUHUDA WA KRISTO

Wapendwa taifa la Mungu, tunatafakari Injili ya Marko 5:1-20 ambapo tunapata simulizi la kuponywa  mpagani mwenye  pepo ambaye alikuwa akiishi makaburini mchana na usiku akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe. Mtu huyu masikini alikuwa hatari kwa watu wengine na kwake mwenyewe kwasababu ya ushawishi wa mapepo yaliokuwa ndani mwake. Alikuwa amefukuzwa na kutengwa na jumuiya yake na kuishi kwenye makaburi kwasababu haikuwezekana tena kumzuia kwa minyororo au aina yoyote ya kifungo, hivyo kila mtu alimuogopa sana.

Ndugu wapendwa, pepo aliyekuwa ndani ya mtu huyu alikabiliana na Yesu Kristo ndio maana anasema, “Nina nini nawe Yesu, mwana wa Mungu aliye juu?  Nakuapisha usinitese” [MK 5:7]. Yesu anamjibu, “Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu” [MK 5:8]. Baada ya kutoka pepo wachafu wanawaingia nguruwe wapatao elfu mbili na kundi lote linatelemka baharini na kufa. Ndugu wapendwa, Yesu aliweka umuhimu mkubwa wa ukombozi wa mwanadamu kuliko nguruwe ndio maana alikubali ombi la pepo kuwaingia nguruwe. Jambo hili la kuponywa mtu mwenye pepo halikuwafurahisha Wagerasi kwasababu wao walijihusisha na hasara ya kiuchumi ya nguruwe kuzama baharini kuliko ukombozi wa mtu huyu masikini, hivyo hawakuwa na chochote cha kufanya na Yesu zaidi ya kumsihi aondoke mipakani mwao.

Ndugu wapendwa, baada ya kuponywa mtu huyu anamuomba Yesu kuandamaana naye lakini Yesu anamwambia arudi kwa watu wa famila yake na kuwatangazia habari njema ya kukombolewa kwake na huruma ya Mungu. Mtu huyu  alikubali na alikwenda  kutangaza habari  njema eneo la Dekapoli lililokaliwa na watu wengi wa mataifa. Kutangaza habari njema huanza na kusimulia habari ya kile Kristo alichofanya katika maisha ya mtu.

Wapendwa, tunaaswa katika Injili ya leo tuwe mashuhuda wa Kristo kwa kumtangaza bila kuogopa au kutafuna maneno wema na fadhili za Mungu anazotutendea katika maisha yetu. Tujifunze kwa mtu huyu aliyeponywa na Yesu ambaye alikuwa shuhuda wa yale ambayo Kristo alimtendea katika maisha yake. Utukufu wa Mungu unashuhudiwa na yale ambayo Kristo anatutendea, hivyo ndugu zangu uthibitisho wa ukristo wetu ni kutangaza  yale tunayotendewa na Kristo. Tunatakiwa kuwa mbegu ya kwanza kwa mavuno ya ukristo ambayo yanapatikana baada ya ushuhuda wetu.

Ndugu zangu, ushuhuda wa Kristo lazima uanze na mmoja anayemshuhudia kwa anayo mtendea kama alivyofanya mtu huyu mpagani aliyeponywa na Yesu alihubiri bila kuogopa  eneo la Dekapoli lililokaliwa na watu wengi wa mataifa mambo makuu Yesu aliyomtendea na watu wote wakastaajabu hivyo sote tuna wajibu wa Kusimama imara kumtangaza Yesu Kristo bila kuogopa macho na maneno ya watu.

Tumsifu Yesu Kristo!         

Tafakari hii imeletwa kwenu nami,

Frt Deodatus Mteme

Jimbo katoliki la Morogoro

Mwaka wa pili wa Teologia

Seminari kuu  ya Mtakatifu Paulo  Kipalapala-Tabora.