TAFAKARI YA SIKU JUMATANO YA JUMA LA 4 LA MWAKA 06/02/2019

SCAN OUR NAME TAG TO FOLLOW US ON INSTAGRAM

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU, LEO JUMATANO TAREHE 06/02/2019

Somo: Mk. 6:1-6

Utangulizi

Wapendwa Taifa la Mungu, tumsifu Yesu Kristu. Karibuni katika tafakari ya Neno la Mungu leo tarehe 06/02/2019, Jumatano ya Juma la Nne la mwaka C wa Kanisa. Masomo yetu ya leo; somo la  kwanza linatoka Waraka kwa Waebrania 12:4-7, 11-15, na somo la Injili ni Marko 6:1-6. Karibuni tusikilize somo la Injili.

Somo la injili ilivyoandikwa na Mtakatifu Marko

Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, “Huyu ameyapata wapi haya?” na, “ni hekima gani hii aliyopewa huyu?” na, “Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu?” Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.” Wala hakuweza kufanya mwujiza wowote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Neno la Bwana…

 

 

 

 

Tafakari

Wapendwa Taifa la Mungu, Wazo kuu katika Injili tuliyoisikia hivi punde ni Kukataliwa kwa Yesu. Katika Injili hii tumesikia kuwa Yesu pamoja na wafuasi wake ameenda kuhubiri katika mji wake mwenyewe yaani Nazareth. Na kama ilivyo kawaida kwa Myaudi mwenye imani na ibada, alianza kuhubiri katika sinagogi siku ya sabato. Watu wa mji wake wanashangaa kwa hekima ya ajabu waliyoisikia na kwa miujiza mbalimbali aliyokuwa anaifanya. Na walishangaa kwa sababu walikuwa wanamfahamu Yesu, wazazi wake na ndugu zake. Wanafunga macho na masikio ya mioyo yao na kuacha kumsikiliza Yesu. Nasi pia pengine tumefunga akili na mioyo yetu na kuacha kumsikiliza Yesu, tukidhani kuwa tunamfahamu zaidi.

Wapendwa Taifa la Mungu, pia katika somo la leo tumesikia kuwa baada ya watu kuona wanamfahamu Yesu, “walijikwaa kwake”. Neno hili “kujikwaa” maana yake walimdharau. Na Yesu anawaambia “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake Mwenyewe, na jamaa zake na nyumbani mwake.” (Rej. Mk.6:4). Na hivi watu hawa hawakubahatika kupata mwujiza wowote kutoka kwa Yesu, isipokuwa aliwaponya wagonjwa wachache. Nasi pia kama wabatizwa tunatumwa kutangaza Neno la Mungu kwa ndugu na jamaa zetu. Hivyo wakati mwingine tunakumbana na changamoto mbalimbali kama vile kukataliwa kwa vile tunafahamiana na wale tunaowahubiria. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba sisi hatupo tofauti sana na watu wa Nazareti. Kilichotokea kwa watu hawa kinaweza hata kikatokea kwetu. Maana daima Mungu anaongea nasi kwa njia ya watu tunaowafahamu, matukio na hali mbalimbali za maisha yetu ya kila siku. Lakini hatuitambui sauti yake au ujumbe wake kwa sababu anaongea nasi kupitia mtu ambaye tunamfahamu, ambaye hatumpendi au ambaye ni mgeni kabisa kwetu. Hivyo tunafunga kabisa milango ya kupata neema na baraka mbalimbali ambazo tungeweza kuzipata kutoka kwa Mungu kupitia watumishi wake. Hivyo basi, Kila mmoja wetu ajiulize ni mara ngapi nimezuia upendo wa Mungu na nguvu yake ya kuponya kwa sababu nimekataa kumpokea yeye mwenyewe kupitia watumishi wake? Kumbe basi, tujichunguze kama tunafanana na watu hawa wa Nazareti, na tufanye mabadiliko ndani mwetu na tuwapokee Manabii wa kweli wanaotumwa kwetu kutuletea habari njema ya Wokovu; ili milango ya neema na Baraka mbalimbali ifunguliwe katika Maisha yetu.

Ndugu zangu, leo pia Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya watakatifu Paulo Miki na wenzake, Mashahidi. Watakatifu hawa walijitahidi sana kuhubiri neno la Mungu kwa bidii na kupata ufanisi mkubwa, na hivi walikataliwa na watu wao wenyewe. Hivyo yeye na wenzake walikamatwa na kuteswa vikali sana. Walikatwa masikio yao ya kushoto na walipitishwa katika miji mbalimbali, damu zikiwa zinachuruzika katika mashavu yao ili kuwaogopesha watu. Baadaye walifungwa kwenye misalaba kwa kamba na minyororo mikono na miguu, pamoja na kosi za chuma shingoni mwao. Lakini kutokana na imani kubwa waliyokuwa nayo kwa Bwana wetu Yesu Kristu walikubali kupokea mateso hayo makali na kuuwawa msalabani. Hivyo basi tumwombe Mungu ili kwa maombezi ya watakatifu hawa, atupe nguvu ya kutangaza neno lake popote, tusiogope watu, matukano, mateso wala kufa. (Rum. 8:38-39). Kwa kufanya hivyo, tunadhihirisha ufalme wa Mungu hapa duniani na hivi kufanya watu wote wamjue, wampende, wamtumikie Mungu tuwapo hai hapa duniani  na Mwisho tukifa tufike kwake Mbinguni na tufurahi pamoja naye milele.

Tumsifu Yesu Kristu….

Tafakari hii imeletwa kwenu na Frt. Deogratias Arumasi.

Wa Jimbo Katoliki Moshi,  Mwaka wa Nne Teolojia katika

Seminari Kuu ya Kipalapala-Tabora

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.