TAFAKARI YA SIKU JUMANNE YA JUMA LA 4 LA MWAKA C WA KANISA 05/02/2019

WAZO KUU NI WITO WA MUNGU KATIKA MAISHA YETU.

Wapendwa Taifa la Mungu, Tumsifu Yesu Kristo!

Leo ni Dominika ya 5 ya Mwaka C wa Kanisa. Ikiwa pia ni siku ya kumbukumbuku ya Mtakatifu Skolastika, Bikira.

Masomo ya leo:

Kitabu cha Nabii Isaya 6:1-8

Waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorinto 15:1-11

Injili ya Mtakatifu Luka 5:1-11          

Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mtakatifu Luka

1Ikawa Makutano walimsoga wakilisikiliza Neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, 2akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao. 3 Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chumboni.

4 Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, “Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.” 5 Simoni akajibu akamwambia, “Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.” 6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; 7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. 8 Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.” 9Maana alishikwa na mshangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; 10 na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.” 11 Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata

 

Neno la Bwana.

Wapendwa Taifa la Mungu, nawaalika tutafakari juu ya WITO WA MUNGU KATIKA MAISHA YETU.

Bwana Wetu Yesu Kristo anawaita wanafunzi wake wanne leo. Kuitwa kwao wanafunzi hawa kunatupatia Dhima hii ya WITO wa Mungu katika Maisha yetu. Wito huu ni wa pekee maana unatoka kwa Mungu.

Katika somo la kwanza Nabii Isaya anaitwa kwa namna ya pekee na Mungu, anaposema, “nimtume nani…?” (Isa 6:8) naye anaitikia, “mimi hapa, nitume mimi!” (Isa 6:8) na hivyo tunaliona wazo la Wito katika maisha ya nabii Isaya.

Mtakatifu Paulo pia anaonyesha wito wake ulivyotoka kwa Kristo katika 1 Kor 15:8 akisema “na mwisho wa wote alinitokea mimi” kuonyesha namna alivyopewa mwito na Bwana Yesu wa kuhubiri habari njema.

Wito ni sauti ya Mungu kwetu inayokuja na wajibu na inahitaji utayari wetu ili kufanya kazi ndani yetu. Mfano Mzuri ni wanafunzi hawa wanne wanaokuwa tayari kuacha vyote na kumfuata Bwana wetu Yesu Kristo. Pia mfano mwingine, Ni Mtakatifu Paulo ambaye tangu alipopokea wito wa kuhudumu aliendelea kufanya hivyo.

Wito katika maisha yetu huambatana na Neema za Mungu ambazo tunapaswa kushirikiana nazo. Mfano mzuri ni Mtakatifu Paulo anayesema waziwazi kuwaLakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo … wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.” 1 Kor 15:10.

Tutafakari wito wa Mungu kwetu katika Makundi matatu: yaani, wito wa kuwa Mwanadamu, wito wa kuwa Mkristo na pia wito wa kuwa Mwana Ndoa, Padre au Mtawa.

Kundi la kwanza la Wito wa kuwa mwanadamu unatokana na kuumbwa kama Mwanadamu na sio kitu kingine. Wito huu unatupatia wajibu wa kuitunza na kuitiisha dunia. Kuyatunza mazingira, kuutunza Uasili wa dunia, kuutunza Uasili wetu na kuishi kama Wanadamu na sio wanyama au kitu kingine chochote.

Kundi la pili la Wito wa kuwa Mkristo unatupatia wajibu wa kuuishi upendo. Kumpenda sana Mungu kuliko yote, yaani chochote kingine kikija Mungu awe na nafasi ya kwanza. Tuwapende Jirani zetu kama Nafsi zetu. Upendo wa Nafsi zetu na wa Jirani zetu usizidiane kwa namna yoyote, yaani uwe katika uwiano sawa.

Na kundi la tatu la Wito wa kuwa Wana Ndoa, Mapadre au Watawa una wajibu wa kuyaishi mashauri ya Injili ambayo ni: Usafi wa Moyo, Utii na Ufukara. Usafi wa Moyo, unatualika kuwaza, kunena na kutenda yanayotupatia muunganiko na Mungu wakati wote wa maisha yetu, Mfano Mtakatifu Skolastika ambaye leo ni kumbukumbu yake alijitoa kabisa katika ubikira wake kuishi katika Muunganiko na Mungu, Utii, unatuwezesha kutambua mipaka ya uwezo wetu na kuwa wanyenyekevu, hivyo unyenyekevu unatuwezesha kuwa  na Utii kwa Mungu, Mamlaka halali na kwa Dhamiri zetu hai, na Ufukara, ni Kujitolea na kumtolea Mungu yote tuliyonayo na kutokuwa na chochote kinachoweza kututenganisha Naye.

Wapendwa Taifa la Mungu, kama Wanafunzi walivyoacha vyote na kumfuasa Kristo tunapaswa kumfuasa Yesu Kristo kwa kushika mafundisho yake, kushika amri zake, kuishi maisha ya Fadhila, kuishi maisha ya unyenyekevu, maisha ya toba na kuikimbilia Huruma yake siku zote.

Lakini pia kwa namna ya pekee tunaalikwa wote kuacha tamaduni zinazohatarisha wajibu wetu wa kuitunza dunia, ambao ni wito wetu wa kuwa binadamu. Kwa mfano, kuchoma misitu na kukata miti bila kupanda ni kwenda kinyume na makusudi ya Mungu ambaye alimtwaa “huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” (Mwanzo 2:15) Ni kuilima na kuitunza na sio kuiharibu.

Na pia kuacha tamaduni hatarishi za kuuishi upendo. Kwa Mfano, Utoaji mimba na matumizi ya sayansi na teknolojia kumaliza uhai kwa namna yoyote ambako ni kushindwa kuishi wito wetu wa Ukristo, ambao wajibu wake ni upendo  na kutunza maisha ambayo ni zawadi ya Mungu kwetu, kama inavyoelezwa katika Mwanzo 2:7, isemayo “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Hivyo tunapaswa kuyatunza maisha yetu na ya wengine pia.

Na tena kuacha tamaduni hatarishi zinazopelekea kushindwa kuyaishi mashauri ya Injili ambayo ni usafi wa moyo, utii na ufukara, kwa mfano, Mwanandoa kuishi bila kumjali mwenzake, kujali matakwa yake tu, na kumchukulia mwenzake kama mashine ya kumkamilishia yanayopungua. Lakini pia Padre au Mtawa anayekimbia wajibu wake, anayetaka kuishi bila ya kujali na anayewakwaza tu anaowahudumia anashindwa kuishi wito wake pia.

Wapendwa Taifa la Mungu, ni wajibu wetu kuyafanya maisha yetu yafungamane na wito tunaopewa na Bwana wetu Yesu Kristo katika injili ya leo, ambao ni wa kuwa wavuvi wa watu kwa namna zetu mbalimbali. Maisha yetu yautambulishe wito wetu na wito wetu utambulike kwa Maisha yetu.

Mama Bikira Maria Atuombee daima katika maisha yetu ili tuweze kuitikia wito wa Mungu daima katika maisha yetu kama yeye alivyofanya aliposema, “Tazama, mimi ni  mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38)

AMINA

Tafakari hii imetolewa na mimi,

Frt Dietrich Kapufi, Jimbo Katoliki la Kigoma.

Mwaka wa Pili wa Teolojia, Seminari kuu Kipalapala – Tabora.

 

Tumsifu Yesu Kristo!

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.