TAFAKARI YA SIKU IJUMAA YA JUMA LA 2 LA KWARESMA MWAKA C 22.03.2019

TAFAKARI YA SIKU YA IJUMAA JUMA LA 2 LA KWARESMA

Somo 1 Mw. 37 : 3 – 4, 12-13, 17 -28.

Zab. 105 : 16 – 21

Injili. Mt 21 : 33 – 43,45-46.

Wapendwa taifa la Mungu Tumsifu Yesu Kristu…..,

Tupo katika kipindi cha mfungo wa Kwaresma ambacho kwacho Mama Kanisa anatuasa tujirudi, tuchunguze dhamiri zetu, tufanye toba ya kweli ili tuweze kupata neema kutoka kwa Mungu. Wapendwa ndugu zangu karibuni tutafakari ujumbe wa Mungu tuliousikia hivi punde kutoka kwa mwinjili Mathayo.

Tunaona Yesu akitumia mfano wa shamba na mkulima, kuelezea ukweli juu ya maisha yetu. Mwenye shamba tunaweza kusema ni Mungu mwenyewe ambaye anatubariki, anatulinda na kutujalia neema zake kama mwenye shamba  alivyoandaa vizuri shamba lake la mzabibu. Shamba la mzabibu ni taifa teule la Bwana la  Israeli ambalo kwetu sisi  wakristu ndilo chimbuko letu,  na watumishi wake ndiyo manabii, anawatuma kwetu sisi kutuletea  ujumbe  wake,  lakini hatuwasikilizi bali tunawapinga na kuwaua kama ambavyo walivyofanya wale wakulima ambao hawakuwa waaminifu,  rejea(1fal  19:10 ), (Yer 20:2 ), (Mt 5:12 )

Kama vile haitoshi bado, Mungu anamtuma mwanae wa  pekee kwetu sisi, rejea (Yoh 3:16 ) lakini pia tunampinga na kumuua, hivyo Mungu atatuadhibu sisi sote ambao hatuko tayari kumkiri na kumwamini  Yesu Kristu kuwa ni Bwana na Mungu wetu, rejea (Zab 118:22–23 ), Yesu Kristu ni jiwe la msingi ambalo lilikataliwa na waashi rejea (1Pet 2 : 4–8). Hivyo tukimpinga na kutomkubali Yesu Kristu Kanisa litakabidhiwa kwa watu wengine wachaMungu ambao kwa macho yetu tunaweza kuona hawastahiri, rejea (Efe 2:19 ).

Ziko dhamiri kuu 3 tunazojifunza kupitia somo hili  :-

  1. Huruma ya Mungu kwetu sisi,
  2.  Tunaonywa tuwe watu wa shukrani na tuache ubinafsi,
  3.  Tukubali kuambiwa ukweli na kurekebisha vilema vyetu.

Wapendwa ndugu zangu Mungu ni mwenye huruma na hapendi tupotee hivyo anatutumia manabii, wahubiri wajumbe wa neno lake, ili kupitia hao tuweze kubadilika na kuacha matendo maovu. Katika somo la leo tumesikia mwenye shamba akiwatuma watumishi wake kwenda kuchukua sehemu ya mavuno yake bila kuchoka ingawaje watumishi wake walipigwa na kuuawa.

Injili ya leo inatuasa

  1. Tuwe watu wa shukrani na tuache ubinafsi, Mungu ametujalia vipawa mbalimbali hivyo tuvitumie vipawa hivyo  sio kwa ajili yetu tu, bali kwa ajili ya wengine.
  2.  Tuwe wepesi katika kutoa sadaka, zaka na mavuno ikiwa ni sehemu ya shukrani kwa Mungu wetu.
  3. Tumesikia katika somo la Injili wakulima wasio waaminifu, sababu ya ubinafsi wao waligoma kutoa sehemu ya  mavuno kwa bwana wao na kutaka kujibinafsishia shamba ambalo sio mali yao na kuwaua watumishi waliotumwa kwa ajili ya kuchukua sehemu ya mavuno na adhabu yao ilikuwa ni kuangamizwa; hivyo tuone ni jinsi gani Mungu anachukizwa sana na tabia hiyo.
  4. Wapendwa ndugu zangu tukubali kuambiwa ukweli na kurekebisha vilema vyetu.Tumesikia katika somo la Injili kuwa makuhani wakuu, na wafarisayo waliposikia hiyo mifano ya Yesu walitambua kuwa wanasemwa wao, hivyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni; vilevile na sisi tunaweza kuwa na tabia ya kuchukia watu na kutaka kuwadhuru wale ambao wanatuambia ukweli na kukemea matendo yetu maovu.

 

Kwa hiyo basi ndugu zangu wapendwa, sisi kama wakulima waaminifu katika shamba la mzabibu la Bwana ambalo ndiyo Kanisa, tufanye kazi kwa bidii, kwa kuishi maisha ya utakatifu , kuishi vizuri kwa kuyatimiza matakwa ya Mungu ili tuweze kupata mavuno mengi  katika shamba la Bwana,nasi wenyewe hatimae tupate thawabu ya kuwa mavuno ya milele na kuhifadhiwa katika ghala lake mbinguni miongoni mwa watakatifu.

 

Tumsifu Yesu Kristu….!

 

TAFAKARI HII IMELETWA KWENU NAMI FRT JAMES MOGELLA,

KUTOKA JIMBO KATOLIKI MOROGORO,MWAKA WA KWANZA WA TEOLOJIA KATIKA SEMINARI KUU YA MT. PAULO KIPALAPALA TABORA.

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.