TAFAKARI YA SIKU JUMATATU YA JUMA LA 4 LA KWARESIMA MWAKA C 01.02.2019

TAFAKARI YA LEO – JUMATATU 01/04/2019, JUMA LA 4 LA KWARESMA

“MUNGU NDIYE ASILI YA UZIMA WETU”

(Yn 4:43-54)

Wapendwa Taifa la Mungu napenda kuwakaribisha katika tafakari hii fupi ya Somo la Injili tuliyoisikia hivi punde. Awali ya yote, Mwinjili Yohane anamtambulisha Bwana wetu Yesu Kristo kwamba ni Neno la Mungu ambaye alikuja duniani, akawa mwanadamu, akakaa kwetu bila dhambi (Yn 1:4). Lengo kuu la ujio wake hapa duniani na hata kuishi miongoni mwetu ni kuihubiri Injili ya furaha na amani ambayo kwayo ni chimbuko na kiiini cha Wokovu kwa wote waisikiao na kuiamini hata wapate uzima wa milele.

Wapendwa Taifa la Mungu, tunapoendelea na Mfungo wetu wa Kwaresma, leo Bwana wetu Yesu Kristo anamponya binti aliye katika hatari ya kufa. Kifo huleta kupungukiwa, huzuni na majonzi kwa jamaa za marehemu. Kwa sababu ya huruma na upendo wake mkuu kwa wanadamu, Kristo anamrudishia uzima binti huyu na hivi kurudisha furaha na amani kwa jamaa yake yote, furaha ambayo ilikwisha anza kutoweka kwa sababu ya ugonjwa uliohatarisha maisha yake. Kumbe Kristo ndiye Bwana wa uzima!

Wapendwa Taifa la Mungu, Mungu ndiye asili ya uzima wetu sisi wanadamu. Yeye ndiye anayetujalia afya ya mwili na roho na kuturudishia nguvu pindi tupitapo katika majaribu ya kiroho na kimwili yanayodhoofisha uzima wetu. Tunapaswa kumkimbilia Yeye kwa njia ya sala kila tunapokumbana na vihatarishi vya uzima wa roho zetu hasa vishawishi vya dhambi, kama ambavyo huyu afisa alivyomkimbilia Kristo ili binti yake apate kuponywa na kurudishiwa uzima wake.

Wapendwa Taifa la Mungu, tukisukumwa na moyo wa Imani, sisi sote hasa Wabatizwa kwa namna ya pekee, tunapaswa kuwa waenezaji wa amani na furaha sio tu katika familia na jumuiya zetu, bali pia kwa jamii nzima ya wanadamu popote pale tulipo. Tuwarudishie tena uzima wale wanaoupoteza kwa kukata tamaa ya maisha, walio katika mafarakano na vita, masikini wanaohitaji msaada wetu na wanaoteseka katika magonjwa. Pia turudishe uzima katika ndoa na mahusiano yetu na wengine. Tuwape matumaini na kuwatia moyo wale wote walio katika dhambi, kwa kuwahimiza kupokea Sakramenti ya Kitubio ambayo ni Skramenti ya Uponyaji.

Wapendwa Taifa la Mungu, tumwombe Mama yetu Bikira Maria aliyekuwa wa kwanza kumpokea Bwana wetu Yesu Kristo katika Fumbo la Umwilisho na hivi kuwa wa kwanza pia kuipokea Imani (Lk 1:26-38), atuombee kwa Mwanae ili atuongezee Imani, Imani ambayo inaponya na inatujengea mahusiano bora na kutupatia uzima kutoka kwa Mungu wetu. Uzima huo utatustahilisha kuurithi uzima wa milele mbinguni. Amina