Injili, mshikamano matunda ya ukristo miaka 150-Kard. Pengo

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema kuwa katika kuadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara Kanisa linajivunia kuenea kwa injili sehmu mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki na kubainisha kuwa matokeo ya maadhimisho hayo kuimarika kwa muungano kati ya watanzania

Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 17, 2018 wakati huu ambapo Kanisa lipo katika maandalizi kuelekea kilele cha maadhimisho ya jubilei hiyo itakayofanyika Novemba 2 hadi 4 Bagamoyo, Jimbo Katoliki Morogoro.

ÔÇ£Maadhimisho ya jubilee hii tunatamani matokeo yake yawe kuimarika zaidi kwa uinjilishaji kwanza, lakini vile vile yalete muungano kwa wananchi wote licha ya tofauti tunazokuwa nazo za kidini na kiimani. Kwamba tupige hatua zaidi za kuwa wamojaÔÇØameeleza Kardinali Pengo.

Aidha Kardinali Pengo ameweka wazi kuwa Kanisa linapoadhimisha jubilee hiyo lina mengi ya kujivunia kwa kuwa katika muda wote wa miaka 150, ujumbe wa Injili haukubaki Bagamoyo, na wala haukubaki visiwani lakini umeenea mpaka sehemu hizo ambazo kuna wakristo wengi walioipokoea Injili katika nchi mbalimbali Afrika Mashariki.

ÔÇ£Kanisa pia limekuwa ni chanzo cha elimu. Mambo muhimu kama ya kusoma na kuandika yameanzishwa na hawa wamisionari. Tulivyo leo ni kutokana na kazi waliyoianza wamisionariÔÇØ ameongeza Kardinali Pengo.

Pia amesema kuwa Kanisa daima limejitahidi kutoa huduma za kijamii kama afya, elimu na miradi ya kijamii na hivyo kuwawezesha watanzania kupata huduma hizo bila ubaguzi, hasa katika sehemu ambazo serikali na taasisi binafsi hawakufika kutoa huduma hizo.

ÔÇ£ Kuna sehemu ambazo najua mpaka miaka michache iliyopita hakukuwa na hospitali za serikali wala watu binafsi zaidi ya huduma zilizotolewa na Kanisa KatolikiÔÇØ amesema.

Akielezea sababu za maadhimisho hayo kufanyika Bagamoyo Kardinali Pengo amesema kuwa wamisonari wa kwanza walifika Bagamoyo wakaanzisha kituo, na kituo hicho kikawa njia ya kusambaza imani ya kikristo siyo tu Tanzania Bara bali hata nchi jirani, nah ii ndiyo sababu ya kufanyia maadhimisho hayo Bagamoyo

ÔÇ£Mwanzoni wamisionari walipofika walieleweka kuwa nao waliendeleza biashara ya utumwa, lakini wao waliwanunua na kuwakomboa watumwa. Wakaanzisha kijiji pale Bagamoyo kando kando ya eneo walipokuwa wamefika na kusimika msalaba. Walitengeneza kijiji cha Mariam, ndio wakaanza kulea na kuelimisha watu mambo ya kusoma na kuandika, ujenzi, upishi na mambo mengineÔÇØ amefafanua.

Amebainisha kuwa lengo la wamisionari hao waliona kuwa kupitia biashara ya utumwa hata kama ni mbaya kiasi gani inaweza kuwa pia mlango wa kuweza kuanza utume wao katika sehemu hizo.

ÔÇ£Kwa hiyo tayari kule Bagamoyo walikuwa wameanzisha shule za useremala na vituo vya kuelimisha watu ambao walikombolewa na hawa wamisionariÔÇØ amesema.

Pia Kardinali Pengo amesema kuwa uwepo wa changamoto mbalimbali nchini haimaanishi kwamba Injili imeshindwa kukoleza maisha ya watu, bali Injili inafanya kazi yake ambayo inapaswa kwenda sambamba na jitihada za pamoja za wadau wengine wa maendeleo na amani.

ÔÇ£Injili inafanya kazi yake, huwezi ukafikiri kwamba kwa sababu umetamka hili katika misingi ya injili ndo lazima mambo yabadilike ghafla. Injili haiko peke yake kama wadau wa amani na melewanao kati ya watu. Kuwepo kwa changamoto siyo failure (kushindwa) ya Injili peke yake kwa sababu wadau wa amani ni pamoja na serikali, dini na madhehebu mbalimbali. Hakuna dini wala serikali ambayo inataka watu waendelee kuteseka na kukosa amani. Wote tunapigania amaniÔÇØ amebainisha.

Kilele cha jubilei

 

Kilele cha Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara kitafanyika Bagamoyo Jimbo Katoliki Morogoro ambapo Misa siku ya kuwasili Novemba 2, 2018 itaadhimishwa kuombea marehemu wote wakikumbukwa kwa namna ya pekee marehemu wamisionari.

Misa tarehe Novemba 3 itakuwa ni Misa ya Bikira Maria Nyota ya Uinjilishaji na Msimamizi wa Tanzania huku Misa ya Kilele ikitarajiwa kufanyika Novemba 4 ambapo itaadhimishwa misa kwa ajili ya kueneza dini  au misa ya uinjilishaji.


Aidha katika kuelekea maadhimisho hayo kutakuwa na Novena itakayoanza Oktoba 24 hadi Novemba 1, 2018 kwa ajili ya kuombea mafanikio ya kilele cha Maadhimisho ya Miaka 150 ya Unjilishaji Tanzania Bara, kuomba uimarishaji wa imani, moyo wa umisionari na ushuhuda wa maisha na kuiombea Tanzania amani.