Benki ya Biashara ya Mkombozi yazindua tawi la Tegeta

Tawi hilo lilifunguliwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa katika hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali, wafanyakazi na wateja wa Benki ya Biashara ya Mkombozi.

Akizindua tawi hilo jipya, Askofu Nzigilwa alisema benki inaendelea kukua vizuri kama ilivyotarajiwa na kwamba malengo ya Benki ya Biashara ya Mkombozi ni kuwa na matawi nchi nzima ili Watanzania wote waweze kupata huduma za kibenki.

ÔÇ£Nachukua fursa hii kuwaomba Watanzania wote kuitumia  benki hii. Hii ni benki  inayomilikiwa na Watanzania wenyewe kwani mpaka sasa hakuna pesa yeyote iliyowekwa na mwekezaji yeyote wa nje,ÔÇØ alisema na kuongeza kuwa ufunguzi  wa tawi hilo la Tegeta ni udhihirisho wa dhamira njema ya Benki ya Mkombozi kama mdau muhimu katika uchumi na maendeleo ya sekta ya fedha.

Askofu huyo pia alitoa witokwa Serikali kuendelea kuunga mkono mipango hii ya maendeleo kwani yote hii ipo kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Mkombozi Bw. George Shumbusho alisema kituo cha huduma Tegeta kilifunguliwa  tangu tarehe 23 Julai 2016 na kimepata mafanikio ya kuridhisha katika kipindi hiki kifupi na hata kupata hadhi ya kuwa tawi.

ÔÇ£Benki imepokelewa vema na wananchi wa kada zote ambao wameendelea kujipatia huduma za kibenki toka viunga vyote vinavyozunguka ama kuhusiana na eneo la Tegeta.  Hii imejidhihirisha kwa ukuaji wa kasi wa akaunti mbalimbali zilizofunguliwa na watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali.  Vile vile benki imeweza kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa taasisi mbalimbali na kwa taasisi binafsi,ÔÇØ alisema.

 

 

 

Akizungumza katika uzinduzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya Mkombozi, Profesa Marcelina Chijoriga alisema benki imeona ni vema kukipandisha hadhi kituo cha Tegeta na kuwa tawi kamili ili kukidhi mahitaji ya huduma za kibenki ya wateja.

ÔÇ£Malengo ya benki hii ni kumkomboa Mtanzania katika wimbi la umasikini kwa kutoa mikopo midogo midogo kwa watu binafsi na mikubwa kwa makampuni. Hii ni benki ya watu wote bila kujali itikadi za siasa au dini, alisema.

Hadi sasa Benki ya Biashara ya Mkombozi ina matawi saba na tawi la nane liko mbioni kuzinduliwa Morogoro wiki ijayo.

Mkombozi Commercial Bank Plc ilianzishwa mwaka 2009 na kanisa la Katoliki Tanzania na taasisi zake kwa madhumuni ya kusaidia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kupata huduma za kifedha. 

Ili kutanua wigo zaidi, waanzilishi wa benki hiyo walitoa nafasi kwa watanzania wengine wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji na kuifanya Mkombozi kuwa iliyo orodheshwa kwenye soko la hisa na mitaji.