TAFAKARI YA SIKU ALHAMISI YA JUMA LA 4 LA MWAKA 07/02/2019

TAFAKARI YA MASOMO ALHAMISI YA JUMA LA 4 LA MWAKA C WA KANISA

FEBRUARI 7, 2019

NA FRT. DEOGRATIAS KATAI

Tumsifu Yesu kristo………………………

Wapendwa taifa la Mungu, karibuni katika tafakari ya Neno la Mungu, Alhamisi ya Juma la nne (4) la Mwaka C wa Kanisa. Ujumbe wa Mungu kwetu leo hii unatukumbusha wajibu wa wafuasi wa Yesu Kristu wa kutangaza Neno la Mungu mahali popote duniani.

  1. Somo la kwanza linatoka waraka kwa Waebrania 12: 18-19, 21-24
  2. Somo la Injili linatoka katika Injili ya Marko 6: 7-13

Wapendwa, katika Injili tumemsikia Yesu anawatuma wanafunzi wake wawili wawili waende kutangaza Neno Lake. Tukumbuke kuwa katika mabaraza ya wayahudi ushahidi wa watu wawili ndio uliokubalika kuwa ni wa kweli. Kumbe Yesu anapowatuma wanafunzi wawili wawili wanapaswa kumshuhudia kwa watu; kwa maana idadi yao hii inathibitisha ukweli wa Kimungu wanaoutangaza. Pia anapowatuma wawili wawili anaonesha kuwa utume si kitu binafsi bali una tabia ya kijumuiya. Unahitaji kutekelezwa kwa ushirikiano kwa kuunganisha nguvu na karama ambazo Yeye mwenyewe anamjalia kila anayemtuma.

Pia Yesu anawapowatuma anawapa msharti ya kufuata huko waendako ili waweze kutekeleza vema kilicho mbele yao. Katika masharti hayo ana wazuia kuchukua vitu vya njiani, anawazuia kubeba mkoba, chakula na pesa. Kwa waisrael walikwisha elewa tayari kuwa Walawi walikotoka makuhani hawakupewa eneo na hawakuwa na mashamba, riziki yao ilipatikana madhabahuni walipohudumu. Hawa pia Yesu anawatuma wakapate mahitaji yao kwa hao wanaokwenda kuwahudumia. Kumbe Yesu anaona Ujumbe  wake niwa muhimu na haraka  na hivyo anatoa mwongozo  kwa wanafunzi wake wakupunguza mizigo wasije wakachelewa njiani  au wakajishughulisha zaidi na mambo mengine yaliyo kinyume cha utume wao au wakasongwa na mahitaji yao wenyewe.  Badala yake anawapa uwezo dhidi ya pepo wachafu na kuponya. Na ujumbe wanaobeba ni mwaliko watu watubu kwa kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Anawaruhusu pia, kuchukua fimbo kama ishara ya mamlaka ambayo kwayo wamepewa na siyo kujitwalia wenyewe.

Wapendwa, Lengo la Yesu kuwatuma wanafunzi wake ni kutoa nafasi kwa watu wengi ilivyowezekana wasikie Ujumbe wake, hasa masharti ya kuingia katika Ufalme wa mbinguni na hatimaye wafanye uamuzi. Pia Kristu anapowatuma wanafunzi wake anaturudisha kwenye asili ya utume na kutuonesha kuwa asili ya utume ni Mungu mwenyewe; ndiye anayeita na kutuma (Ebr. 5:4).

Kumbe wajibu wa kwanza wa yeye anayetumwa na Mungu ni kuwasaidia na kuwaongoza watu ili waufikie Utakatifu. Huu ndio wajibu wa mtume na wajibu wa Kanisa zima. Yesu anatuita sasa kama kanisa kila mmoja kwa nafasi yake akauhubirie ulimwengu Habari Njema ya wokovu. Tukumbuke wazi kwamba tulifanyapo jambo hili kwa uaminifu mambo hayawezi kwenda sawa kila wakati. Tutegemee upinzani na wakati mwingine hata kukataliwa. Na Yesu kwa kuliona hilo anawaambia wanafunzi wake, “na mahali popote wasipowakaribisheni ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao.”

Tuombe Neema ya Mwenyezi Mungu ili itupatie nguvu na ujasiri wa kulitangaza Neno Lake kwa maneno na matendo yetu mema. Pia, tuombee leo utume wa umisionari wa Kanisa ili uweze kuzaa matunda. Mungu atubariki na kutuongoza kwenye utume anaotuitia kila siku.

Tumsifu Yesu Kristo…

Tafakari hii  imeletwa kwenu na  mimi Frt. Deogratias Katai, wa  Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza. Mwaka wa nne wa Teolojia katika Seminari  kuu ya  Mt. Paulo, Kipalapala Tabora.